SEHEMU YA 03
Usiku wa manane…
Yalikuwa malori mawili makubwa, moja lilikuwa na askari na linguine lilikuwa tupu, wakatelemka kuanza kuvamia mazizi ya mifugo, wakaanza kuswaga ng’ombe na mbuzi kupakia katika lori lililo tupu, huku wengine wakianza kuvunja milango ya nyumba. Askari mmoja aliyekuwa akivunja mlango kwa teke alichomwa mshale wa mgongo na kupiga yowe la nguvu, hapo waligundua kuwa kuna watu nje wenye silaha, wale wavamizi wakavamia machaka ya migomba kuanza kusaka huku wakipiga risasi kila wanayemkamata. Mzee Rutashobya alimlenga mmoja aliyeonekana kimbelembele kwa kutoa amri hizo, akamlega na gobole lake akafyatua shabaha safi, ikapasua kichwa cha Yule mtu, kisha akahama kile kichaka na kwenda kichaka kingine ikiwa ni moja ya kuwapoteza wale wavamizi. Mara risasi kama mvua zikakata na kutengeneza uwanja katika lile eneo ambalo risasi ya Rutashobya ilitokea.
“Atakuwa ameshakufa huyo!” mmoja wa askari akasema, lakini kabla hajatoka eneo lile, gobole la Rutashobya lilifanya kazi nyingine likamtungua Yule aliyekuwa akisema hayo, akajibwaga akiwa kifua chote hakitamaniki. Hali ikawa mbaya, kiongozi wa wavamizi aliyejulikana kama Mali ya Mungu ambaye muda wote huo alikuwa ndani ya lori akivuta bangi alimua kuteremka na kumsaka huyo anayejifanya mdunguaji. Mpaka yeye aliposhuka tayari vijana wake wanne walikuwa chini bila uhai, wakiwa wamelazwana gobole la Rutashobya. Mali ya Mungu akajua wazi kuwa wanapambana na mtu anayejua anachokifanya.
Kelele za akina mama na watoto ziligubika anga la kijiji hicho, ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia vilitendwa hadharani kwenye mbalamwezi nyeupe. Mzee Rutashobya bado alikuwa akiwaumiza vichwa wale wavamizi huku akiangalia kila linaloendelea, ijapokuwa roho ilimuuma sana, lakini haikuwezekana yeye kujificha muda wote huku akiwasumbua wale wavamizi, risasi zilimwishia akabaki na gobole tu. Wakiwa bado wanamsaka kwenye migomba, mzee Rutashobya sasa alikuwa amejificha kwenye kichuguu. Mmoja wa wavamizi alikuwa akija huku akifuatiwa na wenzake kuelekea nyumba ya Rutashobya, walipofika walivunja mlango na kumtoa mke wa Rutashobya, Joseph naye alishtuka usingizini, akatoka nje kasi ili kumsaidia mama yake lakini teke kali lilimtupa upande wa pili, kitendo hicho kilimfanya Rutashobya kutoka mwenyewe kwa kasi kumkabili Yule askari aliyefanya hivyo, wakakutana ana kwa ana, Yule mvamizi alimuona Rutashobya akija kasi wakati akijipanga na bunduki yake kumlipua alichelewa kwani kitako cha gobole kilitua shavuni na kuvunja taya la jamaa huyo, Rutashobya akavamiwa na askari kama watano na kuanza kupigwa vibaya, wakati huo kiongozi wao Mali ya Mungu akija taratibu kumuona mtu huyo aliyekuwa akiwanyanyasa na tayari alikuwa ameua askari wane kwa risasi zake nne.
“Mwacheni!” sauti ya Malyamungu iliwafanya vijana hao wenye hasira kumuacha Rutashobya akiwa hoi kwa kipigo, wakati huo mkewe akilia kwa kwikwi na Jose ndio hatamaniki.
Mali ya Mungu akamsogelea Rutashobya, akamtazama kwa tuo,
“Wewe ndio unajifanya kujua siyo?”alimwuliza huku akimzunguka, kisha akasimama na kugeuka upande mwingine,
“Mleteni mkewe hapa, lazima niwaue wote wawili kwa mkono wangu huu uliolaaniwa,” alizungumza kwa sauti yake mbaya huku akiupunga hewani mkono wake wa kuume.
“Aaaaaaaaiiiigghhh!!!!” ilikuwa sauti ya mke wa Rutashobya alipokuwa akiburuzwa kuja kwa mumewe. Joseph alikuwa akitazama huku machozi yakimtoka, alitamani kuwaokoa wazazi wake lakini haikuwezekana hakuwa na nguvu za kufanya hivyo, alibaki kajikunyata na kutazama ukatili huo wanaotendewa wazazi wake. Askari mmoja alimuona Joseph pale alipojikunyata akatoka kwenda kumfuata.
“Kimbia Joseph, usirudi nyuma!” mama yake alimgutusha na Joseph alinyanyuka na kukimbia bila kutazama nyuma akipita katika machaka ya migomba, akilini mwake alihisi kuna mtu anayemfuata nyuma kumbe ulikuwa ni mwangwi wa nyayo zake kila zinapotua ardhini, alipogeuka nyuma kuangali huku akiwa kwenye mbio hizo alijibamiza kwenye mti na kuanguka vibaya, damu zilikuwa zikitiririka kwenye jeraha lililotokea pembeni mwa paji la uso wake, akadondoka chini na kupoteza fahamu.
Giza nene lilimchukua Joseph kusikojulikana, alikuwa akisikia sauti za watu ambao walikuwa hawaeleweki wanachokiongea, hakuweza kuona kitu isipokuwa giza lililomzunguka, giza nene kuliko unavyofikiria, mara akaona watu wa kutisha wenye mapembe na ndimi zinazowaka moto kila waachamapo vinywa vyao, zile kelele zikanyamaza, kukawa na kimya kikuu, sasa Joseph alikuwa akisikia sauti ndogo ya tone la maji lililokuwa likianguka kutoka juu na kutua katika dimbwi kubwa la maji, sauti ile ilijirudia rudia, akahisi kiu kikali kimeshika, akainuka kutoka pale alipolala, mbele yake alisimama mtu mwanaume ambaye mkono wake wa kuume alimshika mwanamke, wote wawili walikuwa wakionekana kwa tabu kutokana na giza lile. Mara mwanga mwembamba ukawamulika, walikuwa wamevaa maguo meupe yaliyokuwa yamewafunika hata nyuso zao zisionekane. Yule mwanaume alijifunua uso wake, alikuwa ni binadamu asiye na sura, sura yote ilikuwa imeliwa kama si wadudu basi sijui ni kitu gani.
“Joseph, hivi ndivyo tulivyofanywa wazazi wako,” ilikuwa sauti ile ile ya baba yke ikimwambia maneno hayo, kisha ikaendelea, “Sasa unabaki kwenye ulimwengu wa peke yako, utateseka sana mwanangu lakini roho za babu zako hazitakuacha, lipa kisasi cha damu hii, damu ya mzimu wa Rutashobya haiendi bila malipo”. Mara tone la maji baridi sana likamdondokea Joseph, akakurupuka kutoka katika mzimio huo, na kujikuta peke yake porini. Ilikuwa ndoto kama ndoto ya kutisha ndoto ya kuogofya sana, Joseph alikuwa akibubujikwa na machozi, kijua kitamu cha asubuhi kilikuwa kikimchoma akiwa juu ya umande wa asubuhi, akajinyanyua na kutazama huku na huko, hakuna alichokishuhudia, ni moshi mkubwa uliotapakaa angani, Joseph akashikwa na uchungu akaanza kutimua mbio kurudi kijijini kwao. Baada ya mwendo wa dakika kumi na tano hivi bila kusimama alitoke upande wa nyuma wa kijiji hicho, akakutana na kibao kikubwa kilichoandikwa,
ENEO HILI LIKO CHINI YA SERIKALI YA UGANDA, USIKATISHE.
Joseph akasimama ghafla akatazama na kusoma kibao hicho lakini hakuelelwa sawasawa kilichoandikwa, alitembea taratibu ndani ya machaka ya migomba, akitazama nyumba zilizokuwa zikifuka moshi kwa kuchomwa moto, miili ya watu bado ilikuwa imelala chini na wengine hawakujulikana walipo, aliendelea kuvuta hatua ndogondogo akitazama vizuri, akafika usawa wa ilipokuwa nyumba yao, moto ulikuwa ukimalizia kuangusha mti wa mwisho uliokuwa umeshikilia nyumba hiyo, yote ikalala chini, jivu. Joseph akajitokeza na kuvunja sheria asiyoijua, akasimama mbele ya nyumba hiyo, alipogeuka, mara akasikia kama mtu akikohoa, akageuka huku moyo wake ukifanya paaaaa! Alikuwa ni mtu aliyelala chini kwenye vumbi na jivu, Joseph akamwendea kwa uoga na kumfikia, aliitambua nguo ya mtu huyo, alikuwa baba yake, aliyekuwa na majeraha na damu kila kona ya mwili wake, sura yake ilikuwa imechafuka na kugandwa na damu nzito ambayo ilificha kabisa sura yake.
“Baba!” Joseph aliita. Mzee Rutashobya aliisikia sauti ya mwanane lakini hakuwa na uwezo wa kumuona kwani alikuwa ametobolewa macho, kabla ya kupigwa risasi mbaya ya kifuani, alikuwa akihangaika kupigania roho yake iliyokuwa ikimuacha taratibu.
“Jose! Hauna wazazi, utabaki Yatima, nilikuwa napigania nchi yangu, lakini haikuwa hivyo, utakuwa mtu mzima, tafadhali damu ya Rutashobya isipotee bila malipo, malipo yanayoistahili,” alipokuwa akisema hayo alikuwa akimwagikwa damu nyingi, akijaribu kuinua mkono wake kuonesha kitu Fulani lakini hakuweza.
“Nini baba?” Joseph aliuliza huku akilia kwa uchungu,
“Nyuma ya shimo la ch….o….. chiiiooooo,” Mzee Rutashobya, akarudi ardhini, Roho ikamuacha akatulia tuli, kwa utulivu mkubwa. Upepo mkali ukaanza kuvuma katika eneo lile, vumbi la moto na jivu likasambaa kila mahali.
“Joseeeeeee kimbiaaaaaaa!!!!!!!!!!” alihisi sauti ya mama yake ikimwambia kwa kelele kubwa, Joseph akatimua mbio na kukimbilia kusikojulikana.
§§§§§
Taarifa ya uvamizi huo mbaya kuliko iliyowahi kutokea katika eneo hilo ilifika makao makuu kwenye kitengo chake. Amiri jeshi mkuu alishikwa na masikitiko makubwa juu ya hali hiyo. Alijishika mikono shavuni akiegemeza viwiko vya mikono hiyo mezani huku kifimbo chake akiwa kakibana kwapani, alionekana wazi kuchoshwa na taarifa hizo za kila siku, aliyafunika macho yake kwa viganja vyake kisha akayafikicha kiasi na kutoa ile mikono na sasa akaiweka mezani na kuwatazama wale walioketi mbele yake. Mkuu wa majeshi, Musuguli na wasaidizi wake, wote walibaki kimya hakuna aliyeongea katika mkutano huo wa dharula.
“Mzee, sisi tulishakwambia kabisa kabisa huyu si mtu wa kumwacha hivi, tazama sasa anavyonyanyasa watu wetu!” Yule mkuu wa jeshi akamwambia Mwalimu.
“Nimekuelewa kijana, hata mimi hapa nafikiri nini cha kufanya, maana hii inatisha, anatudharau huyu, anaingia mpaka ndani kwetu akidai ardhi ni yake, anavunja mikataba ya kimataifa juu ya mipaka ya nchi,” Mwalimu alijibu kwa uchungu, akakiweka kifimbo chake mezani na kujiegemeza kwenye kiti chake cha enzi, kiti kilichoibeba nembo ya taifa, akatafakari jamabo, jamabo la kuamua juu ya usalama wa raia wake.
Wakati Mwalimu akivuta muda kwa busara zake huku akitumia mazungumzo kumsihi Nduli huyo aache anachokifanya, wananchi walikuwa tayari wamechoshwa na hali hiyo, kila mmoja alitamanai kumkamata mtu huyo na kumtafuna nyama lakini wote walikuwa wakisubiri amri ya mkuu wan chi, majeshi yalikwishajipanga kwa vita, yalikuwa yakisubiri amri ili yaanze kazi ambayo kwayo ndio maana wamekuwa wanajeshi.
§§§§§
3 Joseph Rutashobya
alianza maisha mapya, maisha pa sin a baba wala mama, hakumuamini mtu, kila
aliyemuona kwake alimuona kama mnyama, kitendo walichofanyiwa wazazi wake
kilimuuma sana na kilimuachia kumbukumbu mbaya moyoni mwake. Aliamua kuishi
peke yake, kila kukicha alikuwa akitembea mwendo mrefu kwenda asikokujua,
matunda ya mwitu na vyakula vya kuomba, wakati mwingine vyakula vya jalalani
vilimsitiri na adha ya njaa. Kutokana na umri wa Joseph ilikuwa vigumu kutafuta
ndugu aliamini kama wazazi wake wameuawa basi kila binadamu mwenye uhusiano na
yeye ameuawa, hali hii ilimfanya mara akimbie mara atembee kwenye barabara
ndefu za vumbi na machaka ya kutisha.Baada ya mwendo wa siku nyingi wa mvua na jua hatimaye Joseph alifika Bukoba Mjini, kwa jinsi alivyokuwa alihitaji kitu japo cha kula au kunywa ili aweze kupoza njaa kali iliyokuwa imemletea udhoofu. Kila duka aliloingia na kujaribu kuomba chochote alifukuzwa kama mbwa, Joseph akaona maisha hayo hayawezi bora kama angekufa pamoja na wazazi wake, akaamua kwenda kwenye magari mabovu ili kujistiri kwa siku hiyo akiwa amekata tama kabisa ya kupata hata chakula, kichwani mwake mawazo mengi yalikuwa yakipita ‘Au nikaibe tu?’ alijiuliza, lakini kila alipotaka kupitisha uamuzi huo alikumbuka maneno ya mama yake siku nyingi nyuma yaliyokuwa yakimwambia ‘Mwanangu hakuna kitu kibaya kama wizi, ni bora ukaomba kama unahitaji kitu, lakini si kuiba, ukiiba watakupiga na kukuua,’ maneno hayo yalimjengea ukuta katika maamuzi yake,
‘Nikiiba nitapigwa na kuuawa,’ aliyaelewa maneno hayo lakini alibaki njia panda kwa sababu hata akiomba alikuwa hapewi wala hapati.
Akiwa njiani kutafuta maeneo ya kujitiri alikutana na watoto ‘wakora’ waliokuwa wakigombana, Joseph akasimama kuwatazama, akagundua kulikuwa na makundi mawili yasiyopatana na kila kundi lilikuwa na kiongozi wake, hakujua ni nini wanachogombea, aliwatazama kwa dakika kadhaa na alipoona sasa wameanza kupigana, Joseph hakuifurahia hali ile, kwa nini wapigane, akawaendea na kusimama katikati yao.
“Kwa nini mnapina nanyi ni marafiki?” akawauliza.
“Toka hapa kwanza we nani hata uingilie ugomvi wetu, nenda zako ukalelewe na mama yako huko, hapa tunaishi nmanunda tupu, tutakumaliza sisi!” walipiga kelele zilizopishana na haikueleweka nani kasema lipi na lipi kasema nani. Joseph akaamua kuondoka na kuwaacha watoto hao, mmoja kati yao akatukana tusi lililomtaja mama, Joseph akashikwa na hasira, akageuka na kurudi akamkamata Yule aliyetukana, ngumi vichwa na mateke vilitawala, mara wenzake wakaingia kumsaidia Joseph hakujali kwani hasira zilimfanya kama kichaa, akawapiga vibaya wote watano, wakakimbia na kumuacha peke yake. ‘Kumbe na mi najua kupigana!’ alijisemea moyoni kisha akavuta hatua fupifupi na kwenda kuketi karibu na jumba bovu moja ambalo lilikuwa hapo jirani na barabara. Usingizi ukampitia, akalala. Aliposhtuka usingizini, akajikuta hayupo peke yake, kuna watoto wa rika lake, wako watatu. Akawatazama kwa zamu.
“Mnataka nini?” akawauliza.
“Sisi tunataka ujiunge kwenye chama chetu,” wakajibu. Jose aliielewa kauli hiyo kwani hata shuleni alikotoka alisikia mara nyingi watoto wenye mtazamo mmoja kujisema kuwa wana chama chao. Akakubaliana nao, wakafurahi sana. Mmoja wao akajitolea kwenda kuleta chakula, Jose hakujua ni vipi na ni wapi, baada ya nusu saa wote walikuwa wamesinzia tena kwa shibe ya chakula hicho mchanganyiko kilichokuja kwenye mfuko wa plastiki.
Joseph Rutashobya akajitambulisha kwa vijana hao kama ‘Joru’ akaingia rasmi kwenye maisha ya ukora, akawa hakamatiki, mhindi gani asiyemjua Joru, kila uchwao watoto wa Kihindi wanarudi nyumbani wakilia, Joru kawapora, hela, chakula chao cha shule na wakileta ukaidi wanapigwa makwenzi. Akimaliza kupora vitu hivyo moja kwa moja alikuwa anavileta maskani na kula na wenzake, lakini pesa alikuwa akificha daima. Hakuna chama chochote cha watoto wa mtaani kilichokuwa hakimjui Joru, kila wanachama wake wakipigwa yeye ndiye anaenda kama mtetezi na kupiga wote atakaowakuta huko. Maisha hayo yalimjenga usugu Joru akawa haogopi mtu wala watu, mara kadhaa alikurupushwa na polisi lakini alikuwa mjanja sana kwani alikuwa akihamisha chama chake kila baada ya siku mbili na kuwaficha mahali pengine, hiyo iliwafanya polisi au wanaomtafuta washindwe kujua yuko wapi.
Siku moja jioni kama kawaida alikuwa katika harakati zake za kutafuta windo, ndipo alipopambana na mtoto wa mwarabu maarufu sana hapo Bukoba mjini. Wakati Joru na wenzake hawana kitu, wameteseka kwa njaa mchana kutwa yeye alikuwa akirusha maandazi kuwapiga njiwa. Hali hiyo Joru ilimuumiza sana, alimtazama sana Yule motto na kisha akawaambia wenzake wamsubiri akamwende, makofi matatu ya mashavuni yalimtia akili Yule motto akampa joru mfuko wa maandazi yaliyobaki na pesa kidogo alizokuwa nazo mfukoni, bahati mbaya alipofanya hayo kulikuwa na polisi aliyekuwa akimuona. Joru na wenzake wakaondoka kwenda maskani kama kawaida.
Usiku wa siku hiyo Josru akiwa na watu wake ndani ya magari mabovu walikuwa wakisikiliza redio, redio ndogo ambayo Josu alimpora mmoja wa watoto wa kihindi hapo mjini. Ilikuwa kipindi cha majira, saa tatu usiku, hotuba ya kihistoria ya Mwalimu Nyerere ilikuwa ikirudiwa redioni, hotuba hii ilimkuna sana akajikuta akishangilia na kupiga makelele ovyo mpaka wenzake wakaamka.
“Joru vipi una kichaa wewe?” wakamuuliza, lakini Joru aliendelea kushangilia na kupiga mbinja, hii haikuwa tabia ya Joru hata kidogo. Lakini siku hiyo alikuwa kama mtu aliyewehuka akili.
********************************************
Itaendelea kesho....
0766974865

Comments
Post a Comment