RIWAYA: RISASI 4

SEHEMU YA 5

4…. rejea MTUKULA JESHINI
Mkuu wa majeshi Shibagenda aliondoka eneo lile na mgeni rasmi na kuendelea kukagua gwaride hilo. Walipomaliza ukaguzi huo wakarudi jukwaani kuungana na wageni wengine ili kupisha gwaride hilo kufanya utaratibu mwingine wa maadhimisho hayo.

“Gwarideeeee!!!! Kulia geuka!” amri ilitolewa wanajeshi wote wakageuka kulia na kupiga mguu chini, kisha viongozi wa gadi mbalimbali wakaondoka katika maeneo yao kwa mwendo wa haraka na aina yake na kusimama mmbele ya vikosi vyao wakisubiri amri nyingine ya kiongozi wao.

“Gwaride litapita mbele ya mgeni kwa mwendo wa pole, na kisha mwendo wa haraka, mbeleeeeeeee tembea!” amri ikatoka, na ngoma laini kutoka kwa kikosi cha bendi ya tarumbeta cha jeshi ikaanzisha wimbo mtamu na kuwafanya vijana hao waanze kutembea kwa madaha na maringo, kila aliyekuwa hapo alitazama miguu ya vijana hao iliyokuwa ikienda kwa ufundi mkubwa, hakika walipendeza, hakika walivutia, hakika waliipamba sherehe hiyo.

“…Wazazi wangu wangekuwepo, siku hii wangeifurahia sana, mama angenikumbnatia na kunibeba kama nilivyokuwa mchanga, angenitemea mate kwenye paji la uso ili safari hii iwe ya Baraka na mafanikio….”

Joru alikuwa akisema moyoni maneno hayo, akiwa anapita mbele ya jukwaa la mgeni rasmi akiwa amegeukia kulia kama ishara ya heshima kwa mgeni rasmi gwaride linapokuwa katika mwendo wa pole. Mawazo ya Joru yalikuwa ni juu ya wazazi wake siku nzima ya sherehe hiyo. Baada ya dakika thelathini gwaride lilikuwa limejipanga tena mbele ya wageni baada ya kumaliza sehemu hiyo ya kutoa heshima.
Watu walikuwa wamefurika katika uwanja huo wakishangilia na kupiga makofi kila vijana hao wanapoonekana kufanya jambo Fulani la ukakamavu, Joru alikuwa akisumbuliwa na kelele za mashangilio hayo kwa maana alijua wazi kuwa hazimhusu yeye.
Gwaride lilikwisha, tayari ilikuwa ni saa saba mchana, mawingu yalilifunika jua na kufanya hali ya hewa kuwa ya kaupepo kidogo uwanja ulibaki kimya na hakukuwa na mtu katikati isipokuwa wageni na raia waliokuja kuwapongeza ndugu zao kwa kuhitimu mafunzo. Muongoza sherehe  alitangaza kuwa sasa ni wakati wa vijana hao kuonesha umahiri wa mafunzo waliyoyapata. Walianza kuonesha aina mbalimbali za mapigano ya silaha baada ya kumaliza hapo yalifuata mapigano ya mikono, umahiri uliooneshwa wa kucheza mitindo ya kungfu na karate iliwakosha watazamaji, muda wote walikuwa wakiwashangilia vijana hao waliokuwa ndani ya mavazi rasmi ya kijeshi. Baada ya hapo lilifuata onesho la mtu mmoja jinsi anavyoweza kuwakabili watu zaidi ya watano, Joru alikuwa ni huyo mtu mmoja, kazi ikaanza, akavamiwa na wenzake wasiopungua watano, Jorun akaonesha umahiri wa kuwapa kipigo kwa mtindo wa Karate, akipangua na kupiga, akijijengea umakini ili asipatwe na shambulizi lolote, mara kwa mara alionekana jinsi anavyobadili miondoko ya mikono na miguu yake na kutoa aina ya ukelele iliyokuwa ikipendezewsha mchezo huo, dakika tatu alikuwa tayari kawalaza wote chini, makofi na nderemo vikatawala.

Likaja onesho la tatu, kijana yuleyule, sasa alitakiwa kupambana na watu wane wenye visu na mapanga hali yeye hana chochote, Joru alitunisha misuli yake kuonesha jinsi mwili wake sasa ulivyokakamaa kimazoezi, akaonesha umahiri wa kukwepa na kupiga kiufundi kisha akawashinda wote wane na kuwalaza chini, akakusanya mikono yake kifuani na kuinama kwa heshima, makofi yalisikika kila kona. Brigedia Shibagenda hakuamini anachokiona kutoka kwa huyui motto wa mtaani, mtoto aliyesumbua mitaa ya Bukoba mpaka Biharamulo, aliyeonekena takataka, aliyelazwa kwenye mabanda ya kuku lakini leo hii alionekana wazi kuwa ni hazina ya JW, Shibagenda aling’amua wazi kuwa mitaani kuna hazina nyingi zinazozurula ovyo bila kuwekewa mkakati, alijikuta akisimama na kupiga makofi ya kumpongeza. Joru alirudi nyuma na kupisha onesho linguine ambalo liliwasilishwa na wengine kwa umahiri mkubwa na wa kisasa. Baada ya maonesho kadhaa kupita, pale mbele pakawekwa tofali na ilitakiwa mtu mmoja aje kulivunja kwa mikono pia kulikuwa na miti iliyowekwa kma magoli ya mpira yote hayo ilitakiwa mtu ayavunje kwa umahiri, mbele ya wote akasimama Joseph Rutashobya, alipoonekana tu mbele ya watu, wote wakaanza kushangilia huku vijana wakipiga mbinja na kutamka Joru, Joru, Joru Joru. Joru akasimama katika msimamo wa mashambulizi huku akibadilisha mwendo wa mikono yake katika mtindo wa kupendeza, akavuta hatua na kuruka hewani kwa mtindo wa aina yake akapiga kile kigogo kwa mguu wake kikapaa juu, Joru alipotua chini akajirusha tena kwa ufundi na kukizabu kwa mguu wake mwingine na kukipasua vipande viwili, alipotua chini moja kwa moja mkono wake wa kulia ulipiga pigo moja juu ya tofali na kulitawanya vipande vipande, Joru aliuma meno mkono wake ukatetemeka,

“Yuko wapi Mali ya Mungu?” aliongea kwa sauti ya chini huku chozi likimtoka kwa hasira. Makofi, vigelegele, nderemo na vifijo vilimfanya Joru ajue kuwa wapo wanaompenda, wapo wanaomhitaji, wapo wanaomthamini katika jamii, alitikisa kichwa kwa masikitiko, akamuomboleza baba na mama yake, akasimama na kutoa ishara ile ile ya heshima na kurudi kukaa walipokuwa wamekaa wenzake.
Ilipotimu saa nane na nusu sherehe ile ilikuwa ikifika ukingoni, ilikuwa ni wakati wa kutoa zawadi maalum kwa wahitimu.
Miongoni mwa wageni waliohudhuri alikuwepo Dr Janeth Ishengoma, huyu aliposikia jina la Joseph Rutashobya likitamkwa kuwa amepata zawadi ya utii, mlenga shabaha mahiri na ukakamavu, alijikuta anashidwa kujizuia, alikuwa akimfananisha kijana huyu na Yule aliyemtoroka nyumbani kwake siku ile alipomkaribisha na kumuwekea maji bafuni maji ya kuoga na aliporudi hakumkuta. Dr. Janeth alimtafakari Joru hakummaliza alimtazama jinsi anavyotembea kwa ukakamavu akipewa zawadi yake huku mashangilio yakiongezeka, Joru, Joru, Joru, Joru…


§§§§§

Turudi nyuma nyumbani kwa Dr Janeth…
JORU alitazama huku na kule hakuona mtu maana usiku ulikuwa mwingi, akaingia mitaani na kutafuta sehemu yenye kichaka na kujipatia usingizi wake hapo huku bado mguu wake ukiwa haujakaa sawa kwa shuruba nyingine.
Joru alitamani kurudi kuishi na watu lakini aliona wazi kuwa siku akipambana na polisi lazima atafungwa kwa maana alikumbuka madhambi mengi aliyoyafanya na zaidi kumbaka binti wa bosi wake hili lilimuumiza kichwa. Alitamani kurudio kwao kijijini lakini bado alipata kumbukumbu mbaya ya matukio yaliyopita, hakutaka kurudi kule kwanza aliamini kuwa kila mtu atakuwa amekwishakufa kama ilivokuwa kwa wazazi wake, ilimpa shida.

Kulipopambazuka hakutaka kuonekana mitaa ile kabisa, alijivuta taratibu huku mguu mmoja bado ukionekana wazi kuwa kuwa haukuwa sawasawa. Alipokuwa akiifuata barabara kubwa pembezoni tu mwa ile kambi ya jeshi ambako alikuwa akitibwa, akaona gari moja ambayo anaijua fika ikipita kwa kasi na mbele yake ikapunguza mwendo, Joru akasimama kuitazama, akaikumbuka, gari ya bosi wake aliyekuwa akimlaza katika banda la kuku, Joru akatabasamu, ‘Watakoma mama zao,’ akajisemea neno hilo la kashfa, kisha akatoa sonyo refu. Akaendelea kuitazama ile gari ikikata kona kuingia mle jeshini, Joru akashtuka, ‘lo, ningelala kwa Yule mwanamke ningekamatika leo, asante Mungu,’ akajisemea kisha akingia zake mtaani kwa upande mwingine, alipokuwa katika kutembeatembea akitafuta wapi anaweza kupata kifungua kinywa, akahisi mtu akimshika bega, Joru akashtuka, moyo wake ukafanya paaaa!

“Joru,” sauti nzito ya kiume ikayafikia masikio yake. Alipogeuka hakuamini macho yake, Kalokola, rafiki yake wa siku nyingi, aliyekuwa naye katika chama kimoja cha mitaani, sasa walikutana baada ya muda mrefu sana kupita, kila mmoja alikuwa baba tosha kwa kupevuka.

“Kalo, upo? Leo imekuwa bahati sana aisee, tangu tuachane sijaonana na mtu yeyote katika chama chetu, vipi jamaa wanaendeleaje?” Joru aliuliza kwa furaha sana.

“Aaaaa siku ile wewe ulipoondoka, na chama kikaishia palepale, mimi siku hizi sipo kule kaka, nafanya kazi ya ufundi magari,” Kalokola akamwambia Joru.

“Aaaaa mwenzangu umeula! Mimi bado natangatanga na mtaa maisha yananisukuma huku na kule lakini naendelea vyema, nilipowaacha nikaja huku Biharamulo na kufanya vibarua lakini waliniuzi nikawafanyia mbaya, yaani hapa mda wowote nitakuwa mikononi mwa polisi,” Joru alimweleza rafikiye kwa kifupi.

“Aaaa Joru, haujaacha tu fujo zako? Nyoka wa kijani, Joru,” Kalokola aliongea huku akimpigapiga mgongoni kisha wote wakaangua kicheko.

“Sasa Kalo, mwenzio hapa hata chai sijapata halafu naumwa si unaona nachechemea mguu huu,” Joru akajieleza.

“Joru, hilo lisikuumize kichwa, wewe ni rafiki yangu sana, unakumbuka uliniokoa kwenye yale mapigano pale Bukoba na wale watoto wakora, siku yetu ya kwanza kukutana na tukakutawaza kuwa mkubwa wetu,” wakacheka tena na kugonganisha viganja vyao.
Kalokola na Joru wakajivuta mpaka kwenye mgahawa wa jirani na kuingia kisha wakaagiza chain a maandazi kila mmoja, wakanywa huku wakiongea mambo mengi yaliyopita, wakibadilishana mawazo ya kila mmoja alivyofika hapo. Joru alivutiwa sana na mapambano aliyopambana Kalokola katika safari yake.

“Yaani Joru, bora uliondoka, haikupita siku mbili, lilitokea vurugu pale mjini tukakusanywa wote, mi nilifungwa miaka miwili ndipo nilipojifunzia ufundi magari huko magereza, nimetoka jela hata miezi saita sijamaliza bado, nimejishikiza ufundi kwenye gereji ya mwarabu mmoja hivi,” Kalokola alimweleza Joru.

“Safi sana Kalo, umefanya jambo jema sana, sasa utafute pesa, upange au ujenge uoe mke uzae watoto na ujenge familia yako,” Joru alimwambia Kalokola maneno hayo mazito huku mkono wake ukiwa umetua juu ya bega la rafikiye nay eye machozi yakimdondoka taratibu.

“Joru, kwa nini unalia rafiki?” Kalokola akamuuliza.

“Siijui kesho yangu, nasubiri kufa kwangu, sidhani kama nina thamani duniani tena, hata nikifa ni manispaa itakayonizika endapo itagundua maiti yangu, kama la, basi nitabaki niliko na mwili wangu kuliwa na fisi au tumbusi,” Joru aliyasema hayo huku machozi yakimtiririka.

“Joru, acha kulia, umesema vyema kuwa kesho yako huijui name nakuhakikishia kesho yako anaijua Mungu, we tulia, sasa una mpango gani?” kalokola alimtuliza Joru na kisha kumtupia swali.

“Nafikiri kwenda kufia Uganda, nataka nikalipize kisasi cha mauaji ya wazazi wangu,” Joru alijibu.

“Joru, unamjua aliyeuwa wazazi wako?” Kalo aktupa swali linguine.

“Namjua na nimemuona, anaitwa Mali ya Mungu, kama yuko hai lazima nikamuue kama amekufa basi nikalikojolee kaburi lake,” Joru alijibu kisha akatikisa kichwa chake, akata andazi na kujimiminia chai yote iliyobaki kikombeni,

“Aaaaaaaaaggghhhhh! Tanzania Tea Blenders, aisee asante sana kwa kifungua kinywa, sasa mi nafikiri tuagane, nahitaji kupumzika,” Joru akamalizia kusema.

“Joru huna pa kupumzika, nifuate, pale gereji kuna magari mengi mabovu nitakutafutia mojwapo upumzike na hatokusumbua mtu,” Joru alikubaliana na nrafiki yake, wakatoka nje ya mgahawa huo.

“Una shilingi mia tano hapo?” Joru akauliza.

“Ipo, vipi?”

“Ninunulie kofia, nijisitiri pia sura yangu isionekane na wabaya wangu,” Joru akamjibu Kalo.

“Ok, kofia gani inakufaa, balaghashia, pama, kapelo, balleti au ipi?” Kalo akauliza kwa kutaja mlolongo wa kofia.

“Haujaitaja kati ya zote, ninunulie ‘Mungu usinione,’ cap,” Joru akajibu.

Joru na Kalokola waliwasili kaytika gereji anayofanyia kazi kalokola, na kama alivyomuahidi akamfungulia mlango wa hiace moja iliyokuwa hapo muda mrefu na kumuweke kiti kwa kulala, Joru akashukuru na kujipumzisha hapo. Joru alibebwa na usingizi mzito ambao hakupata kwa siku nyingi.

“…Umekuwa sasa Joseph, ni wakati wako wa kuanza kile niichokwambia, usione unafanikiwa kukwepa hatari nyingi, ni baba na babu zako wanaofanya hio kwa kuwa wanakulinda ili uilipie damu yao iliyomwagika…”

Joru alikuwa akiota na kuyasikia maneno hayo aliyokuwa akiambia na baba yake katika ndoto hiyo.

“Sawa baba, nitatimiza,” naye alijibu akiwa usingizini.

“….Usikate tamaa Joseph, usiyachukie maisha, njia yako itafunguka muda si mrefu nawe utaliona jua katikati ya giza, latakaloondosha kwako nuru hafifu ya mbala mwezi na kukuangazia kwa mwanga mpya….”

Joru aliitikia tena lakini bado alikuwa katika usingizi mzito sana, akaendelea kuota ndoto mbayambaya na nzuri nzuri, Joru aliota akitembea juu ya daraja kubwa sana mara akawa anasikia mtoto analia, sauti ya kuomba msaada, sauti ya mtoto mchanga, Joru akasimama na na kutafuta wapi mtoto huyo, mara akamuona motto akilia akiwa amelazwa pembeni tu mwa barabara aliyokuwa akipita, karibu kabisa na daraja lile, alimtazama na kutetemeka sana. Akavuta hatua kumsogelea maana huruma iliukamata moyo wake akamfuata motto Yule taratibu na kumyanyua akamkumbatia kifuani mwake, mara akasikia sauti za vicheko zenye mwangwi wa kutisha zikafuatiwa na makofi ya pongezi.

“….Umekuwa mkubwa Joru, sasa una motto mchanga aliyezaliwa muda huu, hakikisha unamtafutana kumpata huyo ndiye atakuwa faraja yako maishani….”

Joru alikurupuka kama mtu aliyegutushwa ghafla akawa anahema kwa nguvu zote kama mbwa aliyekimbia mwendo mrefu. Akashuka kutoka katika ile gari aliyokuwa amelala, akaliendea bomba na kunawa maji na mengine akanywa kisha akajishika kiuno na kutafakari jambo. Alitazama huku na kule hakumuona Kalokola akauliza kwa jamaa waliokuwa pale wakamwambia Kalokola ametoka kuna gari wamekwenda kulichukua lakini hawakujua atarudi saa ngapi. Joru akaamua kuondoka akawaachia ujumbe kuwa atarudi siku ya pili yake.

ITAENDELEA....

0766974865

Comments