RIWAYA: RISASI 4




SEHEMU YA 02

M
geni rasmi wa gwaride lile alifika pale aliposimama Joru, aliyashuhudia machozi yaliyokuwa yakimtiririka usoni, alionekana wazi ana uchungu na kitu, akasimama mbele ya kuruta huyu, akamtazama tena na tena, mkuu wa majeshi aliyekuwa pamoja na mgeni rasmi ndiyo kwanza alimtambua kijana huyo Joseph Rutashobya 'Joru', mkuu wa majeshi alibaki katumbua macho hakutegemea kabisa kama angemuona kijana huyo, akakumbuka miaka mitatu nyuma, jinsi alivyokutana na kijana mtukutu, mpole, Joru, katika mazingira ya kutatanisha.

MIAKA MITATU ILIOPITA
MISITU YA BIHARAMURO
TAARIFA ya duru za usalama ilisema kuwa idadi ya vitendo vya ujambazi imekuwa kubwa, kila uchwao,  mabasi yanatekwa, watu wanaporwa, wengine kuuawa na kubakwa, polisi walifanya kazi kubwa ya kupambana na majambazi hayo lakini walijikuta wakizidiwa kwani majambazi yalikuwa na silaha kubwa za kivita walizozipata kutoka nchi jirani, wakifanya ujambazi na baadhi ya wanajeshi wa nchi hizo sio tu kuteka mabasi bali hata kuvamia maduka na kupora.
Siku moja kulifanyika uhalifu mkubwa, mabasi sita na malori ya mizigo yaliyokuwa yakienda Kagera na Ngala yalitekwa na majambazi hao walipora mali nyingi za thamani, wakawavua nguo abiria na kuwaacha uchi kisha kuwaamuru waimbe wimbo
‘Mtaji wa masikini ni nguvu zake’
Ilikuwa ni aibu ma fedheha kwa watu hao.
Joru akiwa kajificha msituni, juu ya mti, aliyashuhudia hayo yote yaliyokuwa yakitukia kwa kupitia darubini aliyokuwa nayo, aliumia sana lakini hakuwa na msaada. Alitazama kwa uchungu na alijua wazi kuwa akileta tabu lazima watamuua, alijibana palepale na kuendelea kutazama.
Wale majambazi wakamaliza kazi yao wakakusanya kila kitu, wakikung'uta nguo walizowavua wale abiria na kuchukua kila kilicho katika mifuko kisha wakatokomea msituni.
Joru alitulia kulekule juu ya mti akihofia kushuka akijua kwa vyovyote watafikiri kuwa yeye ni mmoja wao. Baada kama ya nusu saa tangu wale majambazi waondoke, polisi walifika na landrover zao aina ya 110, kwa ajili ya kuwalinda raia hao. Waliwahoji juu ya tukio zima jinsi lilivyokuwa, wakasimulia. Baada ya kila kitu kuwa sawa, yale mabasi na malori yaliondolewa eneo lile.


§§§§§
U
siku wa siku ile ya tukio, polisi wakishirikiana na JW, waliuvamia msitu na kufanya msako wa haja, walipekua kila kichaka na vichaka kusaka mali na majambazi hao.
Wimbi la utekaji mabasi lilikuwa kubwa katika mkoa wa Kagera, askari wa jeshi wa nchi jirani walikuwa wakishirikiana na majambazi katika uporaji huo. Wasafiri na wananchi waliilalamikia serikali kwa hali hiyo. Wahusika walisikiliza kilio hicho, wakakaa kikao na kuamua kulivalia njuga swala la ujambazi katika mkoa huo.
Joru alikuwa ndani ya kichaka usiku huo akiwa kajipumzisha, mara akasikia kelele za mbwa na watu wanaoongea, hakufanikiwa kuchomoka kwani mbwa wa polisi walifika katika kichaka hicho, alipojaribu kujiokoa alichelewa, kwa amri moja walimvamia na amri nyingine walimwacha akiwa hoi, wale polisi na wanajeshi wakamtia pingu kijana huyo kisha msako ukaendelea.
Usiku huo walifanikiwa kuwakamata watu 12 akiwemo Joru, wakawakusanya na kuwatembeza kwa miguu kuelekea barabarani walikoacha magari. Kati ya hao 12 kuna walioleta ujeuri njiani, walipigwa risasi na kuuawa kisha kutelekezwa msituni, ilikuwa ni hali ya kuogofya sana kwa Joru, hakutamani kuangalia nyuma.
Mwendo kama wa nusu saa hivi wakafika barabarani na kuwakuta askari wengine, wakawapokea kwa kichapo cha haja kisha wakawaamuru wote kuchuchumaa chini. Kiongozi wa operesheni hiyo akasogea na kumtazama mmoja mmoja kwa sura akimmulika kwa kurunzi yenye mwanga mkali, akafika kwa Joru, akasimama na kumwangalia sana kijana huyu kwa makini.

“Yaani hata wewe ni jambazi?” akamuuliza Joru.

“Hapana afande,” Joru akajibu.

“Sasa unafanya nini huku?” yule kiongozi wa msako alimuuliza Joru,

“Ni stori ndefu sana mzee,” yule kiongozi wa operesheni ambaye alikuwa ni mtu wa makamo alimtazama tena Joru.

“Unaitwa nani?” akamuuliza

“Joseph Rutashobya,” akajibu.

“Haya nambie kwa nini umekuja huku msituni? Ukinambia ukweli nakuachia ukinidanganya nakufunga jela,”  yule askari alimkaripia. Joru alitulia kimya kisha akaanza kulia.             

“Unalia nini?” Yule askari akauliza kwa ukali.                                                                    

“Afande ni stori ndefu nay a kusikitisha sana, huwa siipendi kuikumbuka kwa maana inanitia uchungu” Joru alisema huku bado akilia kwa vikwifukwifu. Yule askari akamtazama Joru kwa jicho la huruma sana, moyo wake ukaingia ganzi akashindwa kuvumilia, chozi likamdondoka hata kabla Joru hajaweza kuongea chochote katika hilo.
Baada ya kujifikiria mara kadhaa, Joru aliinua kichwa na kumtazama Yule askari jeshi, Shibagenda, kisha Joru akajaribu kukumb uka lile tukio la kutisha katika maisha yake akamueleza kisa na mksa way eye kuwa msituni siku hiyo.

1977
Kijiji Fulani huko Mtukula
“Hatuwezi kukubali kunyang’anywa ardhi hivi hivi, ye nani? Kama ninyi mnamuogopa basi mimi simuogopi,” ilikuwa sauti ya mzee Rutashobya katika mkutano wa kijiji uliotishwa siku moja na mwenyekiti wa kijiji hicho.
Suala la Idd Amin kuvamia Tanzania na kudai maeneo Fulani ni ya Uganda huko pande za Kagera lilichukua kasi, ilikuwa haipiti wiki wanakijiji hawa walisikia sehemu Fulani Amin amevamia na kuteka kijiji Fulani, ilikuwa hali ya kuogofya sana iliyokuwa ikifanywa na hao vibaraka wake ambao wakati mwingine walivamia sit u kwa madai hayo bali kupora mali za wanakijiji na hata kufanya unyanyasaji wa kijinsia kama kubaka na kuwapa wananchi mateso makali mwishoe kuwaua. Mzee Rutashobya, hakuipenda sana hali hiyo, alikuwa akiumia sana kila aliposikia taarifa hizo hasa kupitia redio idhaa ya taifa. Alitamani siku moja apambane na watu hao awaoneshe kama kweli yeye alikuwa ni mmoja wa askari wa KR, jeshi la mkoloni, aliyepigana vita ya pili ya dunia kwa upande wa Ujerumani.

“Mzee Rutashobya unasema tu wewe, wakija hapa sijui hata kama utaweza kukimbia,” mzee mwingine alimpinga Rutashobya.

“Sikia wewe mimi si muoga kama kuku, niko tayari kufa, kama kufa nimeshaona wengi waliokufa siwezi kuogopa kufa, nitajisikia furaha kufa kwa ajili ya nchi yangu na si kwa lingine,” alibisha. Mkutano ulikuwa mrefu sana katika kijiji hicho, hoja ikiwa ni jinsi gani ya kukilinda kijiji chao dhidi ya askari wa nduli Amin ambao waliteka na kunyang’anya ardhi ya wananchi kila kukicha.
Si kwamba viongozi wa chama  na serikali kwa ujumla walikuwa hawalijui hilo lakini bado roho ya subira ilikuwa ikitawala roho za viongozi hao waliokuwa wakisikiliza kila agizo kutoka kwa Mwl J.K Nyerere, ambaye ndiye alikuwa Rais na Amiri jeshi mkuu mwaka huo. Baada ya mkutano huo kwisha na kila mtu kurudi katika kaya yake iliadhimiwa kuanzisha ulinzi wa kulinda kijiji chao.
Usiku wa siku hiyo, mzee Rutashobya na familia yake ya mtoto mmoja, Joseph, walikuwa wameketi nje, mkekani, wakiangaziwa na taa ya kandili iliyokuwa kati yao. Mkewe alikuwa akiendelea kuchambua buni alizokuwa amezivuna kutoka shambani wakati Mzee Rutashobya aliketi kwenye kiti chake cha uzee, macho yake yakiangaza huku na huko katika migomba iliyozunguka eneo hilo lote, pembeni yake alikuwa amelaza bunduki kubwa aina ya gobole na risasi kadhaa zikiwa kwenye mfuko wa suruali yake aliyokuwa amevaa, mdomoni mwake alikuwa akivuta kiko huku akimsimulia hadithi mbalimbali za kale na kumfundisha stadi za maisha mwanae pekee Joseph.

“Na wewe siku moja utakuwa mkubwa,” alimwambia mwanawe.

“Na mi nikiwa mkubwa nitakuwa kama wewe?” Joseph aliuliza.

“Ndiyo, tena itabidi uwe mkakamavu sana, uwe mwanaume asiyeogpa kitu kama mimi baba yako, sikiliza mwanangu, mimi baba yako tangu nikiwa mdogo wakati wa ukoloni, nilikuwa najifunza kila kitu kutoka kwa baba yangu, kuwinda, kulima na kila kitu.” Akavuta kiko chake na kupuliza moshi kwenda angani kisha akaendelea kumueleza mwanae,

“Na wewe ujifunze kutoka kwangu, usikubali mtu akuonee hata siku moja, uwe Mtanzania imara, mwana TANU thabiti, hakikisha unaitetea nchi yako katika lolote lile ikiwa hata kufa, kufa, huo ndio uzalendo mwanangu,” Mzee Ruta alikuwa akimwambia mwanane ambaye alikuwa ameduwaa kwa maneno hayo makali.

“Baba, mi mbona naogopa kufa?” aliuliza.

“Kwa sasa utaogopa kwa sababu hujui, lakini ipo siku hautaogopa kufa, mazingira yatakufanya usiogope kufa hata kidogo, lazima uwe mwanaume kweli kweli, hata mi nikikuachia mji huu basi uweze kuutunza na kuulinda maana ndio utakuwa wajibu wako, wewe huna dada huna kaka, upo peke yako kwa hiyo uwe  mkakamavu katika kila kitu, usijione mdogo” Mzee Ruta aliongea huku akimpigapiga mgongoni mwanawe huyo, hata baadaye aligundua kuwa tayari amekwishalala muda mrefu, na maneno yale yalikuwa yakiingia katika ubongo wake kama ndoto ya kutisha sana yenye matukio ya ajabu ambayo Joseph hakuwahi kuyaona maishani mwake.


§§§§§
J
oseph Rutashobya, mtoto pekee wa mzee Rutashobya alikuwa na umri wa miaka tisa wakati alipokuwa akiambiwa hayo yote na baba yake ambaye tayari umri ulikuwa umekwenda, lakini pamoja na umri wake mkubwa alikuwa ni mkorofi na hakuna mwanakijiji aliyekuwa hamjui mzee huyo. Joseph hata shuleni ilikuwa ni vigumu kupewa adhabu kutokana na ukorofi wa baba yake, ijapokuwa yeye alikuwa ni mpole sana asiyependa kuongea na watu, wengi walisema ni tabia ya mama yake, shuleni hakuwa akichangamana na marafiki, daima alikuwa akiambatana na mtoto wa shangazi yake tu, Kemilembe. Daima utawakuta pamoja hata kama si muda wa masomo, ilikuwa ni vigumu wawili hawa kuwatenganisha kiasi kwamba walionekana kama mapacha wanapoambatana.  Si Joseph wala Kemilembe aliyewahi kufikiri kuwa siku moja watakuja kutengana au kutenganishwa, daima katika maongezi yao ya kitoto waliweka ahadi za kuwa wakiwa wakubwa wataishi kama wazazi wao wanavyoishi, kuishi nyumba moja, kulala pamoja, wao kwao ilikuwa ni kama sehemu ya maisha ya ukubwa ambayo walijua wazi kuwa siku moja watayafikia.
Hata wakati Kemilembe alipoanza kuota matiti, alimwambia Joseph kuwa kifua chake kinavimba huku na huku, Joseph alitazama uvimbe huo na kubonyezabonyeza lakini alikutana na vitu vigumu, kwa kuwa Kemilembe aliamini kuwa Joseph anajua mengi kwa kuwa ni mwanaume, alifurahi sana alipoambiwa na Joseph kuwa

“Sasa utakuwa kama mama, utakuwa na maziwa makubwa, tukiwa na mtoto atanyonyamo.”
Joseph mara nyingi alikuwa akimsikia baba yake anavyosikitika hasa asikilizapo redio yake ndogo ya mbao aina ya Phillips iliyokuwa ikimpa habari kila saa nne, saba na kumi ya kila siku. Mzee Rutashobya alichukizwa wazi na yale anayaoyasikia kutoka kwenye chombo hicho kidogo ambacho Joseph aliaamini kabisa kuwa kuna watu ndani wanaoongea.

“Baba kila ukisikiliza humu unakasirika, kwa nini?” Joseph alimuuliza baba yake.

“Mwanangu, dunia hii sijui tunakwenda wapi, kila siku watu wankufa lakini wenye nguvu wanafumba macho,” akamjibu kana kwamba anamjibu mtu mzima mwenye uelewa mpana. Joseph akamkazia macho baba yake akimaanisha hajamuelewa alichomwambia.

“Umeshawahi kumsikia Idd Amin?” Rutashobya akamuuliza mwanawe.

“Ndio, mwalimu ametuambia kuwa ni mtu mbaya sana, anaua watu,” Joseph akajibu huku akionesha huzuni ya wazi usoni mwake. “Sasa kwa nini polisi wasimkamate?” akauliza.

“Aaah Jose, polisi wote wako chini yake, wanamsikiliza yeye,” Rutashobya akajibu.

“Mi ningekuwa polisi ningempiga bastola,” Jose akajibu akiwa hajui anachokiongea.





Siku iliyofuata….

“…Idd Amin akifa, mimi siwezi kulia, nitamtupa Kagera awe chakula cha Mamba…” 

zilikuwa sauti za watu wakiimba kutoka mbali sana. Joseph akiwa na Kemilembe walikuwa njiani kuelekea shuleni alfajiri ya siku hiyo, mikononi mwao walikuwa na fagio pamoja na vidumu vya kuchotea maji kwa ajili ya kumwagili bustani zao za mbogamboga.

“Kemi, unasikia hao wanaoimba?” Jose alimuuliza Kemilembe.

“Ndiyo, kwani ni akina nani?” Kemilembe aliuliza. Joseph akatulia kwanza bila kujibu akisikiliza zile sauti za ule wimbo ulioonekana kumpa faraja kubwa masikioni mwake.

“Unataka kuwajua?” Joseph aliuliza.

“Ndiyo,” Kemi akajibu. Joseph akamshika mkono Kemilembe na kumvutia kwenye majani, wakajificha huku zile sauti zikikaribia pale walipo. Punde si punde kundi kubwa la watu waliogawanyika katika makundi makubwa manne walipita wakikimbia mchaka mchaka. Walikuwa wanajeshi wengi wenye silaha mikononi, wakiwa wamevaa magwanda yao yenye mabaka mabaka yaliyowafanya waonekane kama wadudu, kofia za chuma zilikuwa zimezungushiwa majani mengi na kufanya kama wamebeba vichaka, walikuwa wakiimba kwa jazba na wakipiga mbinja nyingi. Walipokwisha pita, Joseph na Kemilembe wakajitokeza kutoka kwenye lile chaka walilojificha.

“Wanaenda wapi?” Kemilembe akauliza.

“Watakuwa wanakwenda kumkamata Idd Amin,” Joseph alijibu kwa kujiamini kisha wakavuka barabara na kuelekea shuleni.

Watu wa eneo hilo ilikuwa ni kawaida kwao kuona wanajeshi wakipita na kuimba au wakiwa wamejificha machakani wakiwa katika mazoezi ya kivita kutokana na hali halisi iliyopo. Walikuwa katika hali ya utayari muda wote hasa wale wa mpakani, Mtukula.
Mashuleni nako kulikuwa na ulinzi mkali, tahadhari kabla ya hatari.
Mchana wa siku hiyo, masomo yalipokwisha, Joseph na Kemilembe waliwahi kurudi nyumbani tofauti na siku nyingine. Siku hiyo Joseph alifika nyumbani na kumkuta mama yake akiwa ndio kwanza ametoka shambani lakini hakumkuta baba yake. Alimuuliza mama yake kuwa baba yake amekwenda wapi akajibiwa tu amekwenda kijiji jirani hatochelewa kurudi. Joseph alipitiwa na usingizi baada ya shibe ya mchana, akajilaza kwenye kijitanda kidogo kilicokuwapo sebuleni.
Alishtuliwa na sauti ya baba yake aliyekuwa akimsimulia mama yake habari mbaya na ya kutisha kuwa wameokota maiti za watu katika mto Kagera. Mzee Rutashobya alikuwa akiongea kwa huzuni sana na uchungu juu ya hali hiyo. Joseph aliyekuwa amelala kisungura alikuwa akisikiliza yote. Baadae alipoamka hakusita kumueleza baba yake kuwa amekutana na wanajeshi wakienda kumkamata Idd Amin ili wmtupe Kagera aliwe na Mamba. Joseph akamuuliza baba yake kama katika hizo maiti ilikuwepo ya Idd Amin. Baba yake akamtazama kwa mshangao lakini akajua kuwa ni akili za kitoto tu.

Usiku wa siku hiyo wazee wa kijiji kile walikutana pamoja kujadiliana juu ya hali halisi ilivyo kwa usalama wao kwa mara nyingine, ikiwa pia kuweka zamu ya kulinda. Siku hiyo mzee Rutashobya na wengine tisa walikuwa zamu ya kuweka ulinzi. Mzee Rutashobya kutokana na uzoefu wake wa medani za kivita alipokuwa huko ughaibuni katika vita ya pili ya dunia.


“Mnajua tukiwa wazi watatuona kirahisi, hapa ni kujificha kwenye migomba na wengine kwenye mibuni,” alitoa maelekezo kwa wengine, yakaeleweka. Kila mtu akajificha kama alivyoambiwa, hakuna aliyekuwa hamuamini mzee huyo kwa mipango bahati mbaya tu hakuwa kiongozi katika kijiji hicho.


ITAENDELEA....
0766974865

Comments